|
Miongoni mwa yaliyokuwa masharti ya mkataba ule wa amani wa
Hudaybiyah lilikuwepo sharti moja lililowatia uchungu mno waislamu. Na kwa
upande wa pili Makureishi waliling'ang'ania mno. Sharti hili kwa rehema zake
Allah likageuka na kuwa faraja na mlango wa kutokea katika dhiki wa waislamu
wanyonge walioko Makah. Na likawa mwiba mchungu kwa mushrikina waliokamatana
nalo na kulisisitiza kupindukia. Sasa ikawa wao ndio wanaoendesha juhudi za
kutaka lifutwe sharti hili katika mkataba. Na walitangaza wazi kujivua nalo
hata kabla ya mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwa mkataba ule. Hili lilianza pale
Abu Busweir; Utbah Ibn Usayd At-thaqafiy alipokimbilia Madinah akitokea kwa
Makureishi waliokuwa wakimuadhibu na kumtesa kwa sababu tu ya imani yake. Huku
nyuma Makureishi wakawatuma watu wawili kwenda kwa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie. Kumtaka amrejeshe kwao mtu wao huyo, ikiwa ni katika jumla ya
kulitekeleza mojawapo ya masharti ya mkataba baina yao. Mtume wa Allah
alipojiwa na ujumbe huo akasema: "Ewe Abu Busweir, hakika bila ya shaka sisi
tumeshawapa watu hawa kile unachokijua na wala haitufalii sisi katika dini
yetu kufanya usaliti. Kwa ajili hii basi, rudi kwa watu wako". Abu Busweir
akasema: Ewe Mtume wa Allah! Hivi unanirudisha kwa mushrikina wanifitinishe na
dini yangu?", Mtume akamwambia: "Nenda, kwani hapana shaka Allah atakupa wewe
na wanyonge wote walio pamoja nawe faraja na mlango wa kutokana na dhiki na
taabu mzipatazo". Hapo tena Abu Busweir hakuwa na hila ila kuondoka na kurudi
Makah na wajumbe wawili wale waliotumwa kumrejesha. Akaenda nao hata
walipofika mbali hukoo, akafanya hila na kufanikiwa kuutwaa upanga wa mmoja wa
watu wawili wale. Akampiga na kumkatakata nao mpaka akamuua, mwenziwe kuona
yaliyomfika tim akatimua mbio bila ya kuangalia nyuma kujiokoa na kifo
dhahiri. Mbio zake hizo zikakomelea kwa Bwana Mtume, akiwa anatweta na kuhema
kama bata akasema: "Mtu wenu amemuuua mwenzangu",. Abu Busweir akaja nyuma
yake, akamtolea salamu Mtume kisha akasema: "Imetekelezeka dhima yako ewe
Mtume wa Allah na Allah amekutekelezea. Umenisalimisha kwa watu hawa na
ilhali nimejuzuia kufitiniwa dini yangu". Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akamwambia: "Nenda utakako (lakini sio hapa)". Abu Busweir
alipotoweka machoni, Mtume wa Allah akasema: "Ole wa mama yake, hiyo ni fimbo
ya chuma ya kuchokolea moto lau angelikuwa na watu!"
Abu Busweir akaenda mpaka akapiga kambi katika sehemu fulani
ya mwambao wa bahari, baina ya "Iyswi" na "Dhul-Marwah" katika ardhi ya
Juhaynah. Akakaa hapo na kazi yake ikawa ni kuivizia misafara ya biashara ya
Makureishi ipitayo njia hiyo. Kila msafara uliopita mahala hapo aliushambulia
na kupora mali na chakula. Waislamu wanyonge waliokuwa Makah walipozisikia
khabari za Abu Busweir na maneno aliyoambiwa na Mtume. Wakaanza kuchomoka kwa
uficho mkubwa na kwenda kujiunga na Abu Busweir kwenye kambi yake hiyo. Abu
Jandal naye akafanikiwa kutoroka Makah na kwenda kujiunga na wenzake hao akiwa
analiongoza kundi la watu sabini wapamda wanyama waliosilimu. Watu wa makabila
ya Ghaffar, Aslama na Juhaynah na makundi ya mabedui nao wakaja kujiunga na
waislamu hawa katika kambi hii iliyoanzishwa na Abu Busweir. Mtu ambaye Mtume
alishindwa kumpokea Madinah kutokana na kufungwa (kubanwa) na mkataba wa amani
wa Hudaybiyah, nae asikubali kurudi adhabuni na kifungoni Makah. Kambi yake
hii sasa ikawa na watu wasiopungua mia tatu na ili waweze kuendelea kuishi
hapo, wakalazimika kuvamia na kupora misafara ya biashara ya Makureishi
ipitayo hapo. Haupiti msafara hapo ila hutwaa mali yote na kuwaua watu wa
msafara ule walioshindwa kuponyoka na kukimbia.
Kambi hii ya Abu Busweir ni zao na kivuno kilichotokana na
masharti magumu ya suluhu waliyoyaweka Makureishi, ikawa ni mwiba mchungu
uliowakalia kooni Makureishi. Wakahemewa wasijue la kufanya ila kupeleka
ujumbe kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakimuomba kwa udugu wao
awasaidie kutatua tatizo hili. Wakasema: "Sisi hatuna haja tena na watu hao,
ye yote atakayetoka kwetu kuja kwako, basi sasa mzuie (kuwa nae) na hutakuwa
na kosa (kufanya hivyo)". Hapo ndipo Mtume wa Allah alipoandika barua
kumpelekea Abu Busweir na Abu Jandal akiwaamuru kwenda kwake. Na akiwaamuru
waislamu walio pamoja nao kurejea makwao na wala wasizuie msafara wo wote wa
Makureishi utakaopita hapo.
III.
Busara na weledi wa Mtume
wa Allah katika mambo/mipango:
Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa, kadri siku
zilivyopita ndivyo busara na weledi wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-ilivyobainika. Siasa yake makini na uoni wake wa mbali
ulivyodhihirika na kuwakinaisha maswahaba wake na kuwaonyesha kwamba wao
walifanya haraka kuichukia suluhu ile. Suluhu iliyoleta baraka, kheri na
fanaka tupu kwa Uislamu kama dini na mfumo kamili wa maisha na waislamu
wenyewe. Na ikawadhihirikia wale waliokimwa na suluhu hii kwamba Mtume wa
Allah alikuwa sahihi na aliona mbali kuliko wao. Na kwamba alikuwa na yakini
thabiti kwamba Allah Taala hatomtupa mkono na maono yake ndio yaliyokuwa na
kheri kathiri na kufuzu adhimu.
Sayyidina Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-alikuwa akisema:
"Haukuwahi kupatikana ushindi mnono katika Historia ya Uislamu kuliko ule wa
Hudaybiyah. Lakini watu siku hiyo, fikra zao zilishindwa kuyafikia yaliyokuwa
yakijiri baina ya Muhammad na Bwana Mlezi wake. Na waja hufanya haraka na
ilhali Allah hafanyi haraka kama wafanyavyo waja, mpaka mambo yafikie pale
alipopataka. Kwa yakini nilimuona Suhail Ibn Amrou katika Hijjatul-Wadaai
akiwa amesimama mahala pa kuchinjia wanyama. Akimsogezea Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-ngamia wake, nae Mtume akimchinja kwa mkono wake. Kisha
akamuita kinyozi, akaja akamnyoa, nami nikimuangalia Suhail akiziokota nywele
za Mtume na nikimuona anaziweka machoni kwake. Hapo nikakumbuka namna
alivyokuwa akikataa siku ile ya Hudaybiyah kuandikwa
"BISMILLAAHIR-RAHAMAANIR-RAHIYM". Na namna alivyopinga kwa nguvu zote
kuandikwa "Muhammad Mtume wa Allah". Basi nkamuhimidi Allah aliyemuongoza
kwenye Uislamu, naomba Rehema na Amani imshukie Mtume wa Rehema. Ambaye kwaye
ametuongoza na kutuokoa na hilaki".
|