|
III.
Mtume wa Allah ajaribu
upeo wa juhudi yake kuishi kwa amani na Mayahudi , lakini maumbile yao ya
usaliti yaliwashinda.
Hivi ndivyo yalivyokuwa maisha baina ya Mayahudi na majirani
zao waislamu, yalikuwa ni mrorongo wa chuki na mifundo isiyopoa wala kukatika.
Pamoja na yote haya, bado Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakupenda
kujibu uhasama huu wa Mayahudi. Wala hakutaka kulipa uadui atendawao kwa uadui
mfano wake, bali alikuwa akitafuta sana fursa itakayo muwezesha kuleta suluhu
baina yake na wao ili waweze kuishi kwa amani na usalama. Na kamwe Mtume
hakuanza kuwafanyia uadui, bali alifanya kila juhudi iliyokuwa ndani ya uweza
wake kuwaita katika meza ya amani, mapenzi na ushirikiano.
Wakati uongozi wa Mayahudi katika Khaybar ulipotwaliwa na
Useir Ibn Razaam na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatambua kwamba
anafanya maandalizi ya vita. Akaonelea ni vema amuite katika meza ya
majadiliano ya amani, kwa kutaraji kuwa yeye ana upeo wa kuona mbali kuliko
viongozi waliomtangulia. Kwa kuuitika na kuukubali kwake wito huu wa amani,
alikuwa ameiokoa kaumu yake kutokana na moto wa vita uliowaunguza. Mtume
akampelekea ujumbe wa watu thelathini ukiongozwa na Abdullah Ibn
Rawaahah-Allah awawiye radhi. Ujumbe huu ukamuendea Useir katika utawala wake
Khaybar, wakamwambia: "Je, unatupa amani ili tukuelezee lililotuleta?",
akajibu: "Naam, nami nimepata amani kutoka kwenu?". Wakajibu: "Naam", kisha
ndipo walipomsihi aachane na azma ya vita aliyoiweka na kwamba aende kwa Mtume
wa Allah Madinah. Huko ataapishwa na kutawazwa rasmi uongozi wa Khaybar, ili
watu wake wapate kuishi kwa amani na waislamu. Mwanzoni akaonyesha kuuitika
wito huu wa amani, akatoka pamoja na waislamu akiongozana na watu thelathini,
akimkusudia Mtume Madinah. Alipokuwa njiani akajuta na kujilaumu kwa nini
amechukua uamuzi huo wa kumfuata Mtume, akajiwa na fikra za kuwafanyia usaliti
watu aliopeana nao amani. Akaurukia upanga wa Abdullah akitaka kumpokonya na
kumuua kwa kuutumia, Abdullah akalitambua hilo na kumwambia: "Unataka kufanya
usaliti ewe adui ya Allah?". Akamshukia na kumpiga kwa upanga pigo lililo
litenganisha paja na muundi wake. Akaanguka kutoka juu ya ngamia wake na
hakuchukua muda mrefu akafa kutokana na kutokwa na damu nyingi. Hapo waislamu
wakawaendea watu wake walioongozana nao, wakapambana nao na kufanikiwa kuwaua
wote.
IV.
Mayahudi waazimia
kuushambulia mji wa Madinah, Mtume wa Allah awawahi na kuwashambulia kwao:
Sallaam Ibn Miksham aliposhika hatamu za uongozi wa
Mayahudi wa Khaybar baada ya kuuawa kwa Useir Ibn Razaam. Sera yake ilikuwa ni
kuendeleza mapambano dhidi ya waislamu kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.
Namna hivi ndivyo Mayahudi walivyoendelea kuwa na dhamira ya vita, wakipanga
njama za kuwaangamiza waislamu kila kukicha. Wakiazimia kuutokomelezea mbali
Uislamu kwa gharama yo yote imkinikayo. Ilipotimia suluhu ya Hudaybiyah baina
ya Mtume wa Allah na Makureishi na wakakukbaliana kusitisha vita kwaa muda.
Mayahudi wakakata tamaa kupata msaada wa uungaji mkono wa Waarabu katika
kuitekeleza azma na dhamira yao hii chafu. Sallaam akawatangazia wazi viongozi
wa Khaybar kwamba kuna hatari dhahiri inayotishia uwepo wa Mayahudi Madinah.
Na akawaambia kuwa wajibu wao katika kukielekea kitisho hicho ni kuunda kikosi
miongoni mwao kwa kushirikiana na Mayahudi wa Waadil-Quraa na Taymaa. Kisha
wasonge mbele kuelekea Madinah kuwasagasaga waislamu bila ya kutegemea msaada
wa makabila ya Kiarabu katika vita hivi.
Tayari Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa
amekwishaijua dhamira hii ya Mayahudi wa Khaybar. Akaanza haraka kuchukua
hatua za maandalizi ya vita dhidi yao huko huko kwao kabla hawajatoka kuja
Madinah. Miongoni mwa mbinu alizozitumia Bwana Mtume katika kukabiliana na
adui yake ni kumshtukiza adui kabla hajashambuliwa yeye ghafla. Lakini mpango
na mkakati huu Mtume wa Allah ulivuja, kwani Abdullah Ibn Ubayyi - kama
wasemavyo baadhi ya wapokezi - aliwatumia ujumbe Mayahudi wa Khaybar na
kuwaambia: "Muhammad huyoo anakujieni kwa hivyo chukueni hadhari yenu".
Khabari hii ilipowafikia wakaanza kufanya maandalizi kabambe ya kukabiliana na
Mtume waliyeambiwa kuwa anakuja. Wakawa kila siku wakitoka nje ya mji kiasi
cha wapiganaji alfu kumi kwa lengo la kumfagilia Mtume huko huko kabla
hajaingia mjini kwao. Walitoka wakiwa katika maandalizi ya tayari kwa lo lote,
wakiwa na silaha zao, wakawa wanasema: "Muhammad atupige sisi?! Li mbali hilo
mno, li mbali mno hilo!" Wakazitia ngomeni mali na familia zao katika ngome za
"Kutaybah" na askari wakakusanywa katika ngome za "Nitwaah".
|