|
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza vita kwa mtindo wa mzonge akielekeza
mashambulizi makali karibu kabisa na ngome ya adui. Mayahudi nao wakipigana
kufa kupona kuilinda kila shubiri ya ardhi yao, hawarejei nyuma na kuiacha
ardhi yao mateka mikononi mwa waislamu ila kwa kuzidiwa mno. Kila walipojaribu
kutoka ngomeni waislamu waliwashushia kisago cha nguvu, wakawa hawana hila ila
kurudi kimgongomgongo ngomeni mwao kujipatia hifadhi na kujipanga upya.
Mzingiro ukaendelea kwa siku kadhaa na mapambano yakizidi kupamba moto mpaka
waislamu wakakimwa na hali hiyo. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akakaa siku saba akipambana na watu wa ngome hii. Kila siku akimpa
bendera ya vita mmojawapo wa maswahaba wake na kumtuma kwenda kushambulia huko
ngomeni, lakini akirudi bila ya kupatikana ushindi. Hali ikawa hiyo mpaka pale
Allah Taala alipoifungua ngome hiyo kwa mikono ya Sayyidina Aliy Ibn Abi
Twaalib-Allah amuwiye radhi.
Katika mapambano haya yaliyopelekea kutekwa kwa ngome hii,
aliuuawa shujaa wa Mayahudi; Marhab. Huyu alikuwa ni shujaa wa mashujaa wa
Mayahudi, aliuliwa na Sayyidina Aliy katika mubaraza (mpambano wa wawili
wawili). Katika waliouliwa kwenye mpambano huu alikuwemo pia Mahmoud Ibn
Maslamah kaka wa Muhammad Ibn Maslamah. Huyu aliuawa kwa kudondoshewa jiwe la
kusagia wakati alipokuwa amejiegemeza kwenye ukuta wa ngome akijikinga na joto
kali la siku hiyo. Katika kipindi cha mzingiro huu, alikufa kiongozi wa
Mayahudi; Salaam Ibn Miksham akiuacha uongozi kutwaliwa na Al-Haarith Ibn Abiy
Zaynab.
Ngome hii ya Naaim ilipoangukia mikononi mwa waislamu,
Mayahudi wakakimbilia katika ngome iliyokuwa nyuma ya ngome hii. Hiyo ndio
iliyokuwa ngome ya As-swa’ab Ibn Muaadh, wakajipanga tena humo na kutoa
upinzani mkali na wa nguvu kwa waislamu. Wakawaendesha mbio waislamu kama
simba aliyejeruhiwa mpaka wakafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuvuruga mpango wa
mashambulizi wa waislamu. Waislamu wakarudishwa nyuma mpaka mahala alipokuwa
amesimama Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Al-Habaab Ibn
Al-Mundhir-Allah amuwiye radhi-akasimama imara, huku Mtume akiwahimiza na
kuwatia ari ya kupigana waislamu, wakasonga mbele tena wakiwa na nguvu mpya.
Wakapigana kwa nguvu ya imani mpaka wakafanikiwa kuisambaratisha na kuikata
nguvu ya Mayahudi na kuwalazimisha kurudi nyuma na kujifungia ngomeni mwao.
Lakini waislamu wakafanikiwa kupenya ndani, humo kazi ikawa ni moja tu kuua na
kuchukua mateka mpaka wakaitia mikononi mwao ngome hii ya pili ya Mayahudi.
Katika ngome hii, waislamu walipata shayiri, tende, samli,
zeti, asali na vitu vingine vingi. Kabla ya kuiteka ngome hii, waislamu
walikuwa wamekumbwa na janga la njaa kiasi cha kulazimika kula nyama za
farasi. Walipofanikiwa kuiteka ngome hii na kukuta chakula tele, Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akachelea wasije kushughulishwa na ngawira hii
wakasahahu mpambano ulio mbele yao. Akamtuma mtu kuwalingania ya kwamba:
“Kuleni na walisheni wanyama wenu lakini msibebe”. – Yaani msichukue kitu cho
chote kwa ajili ya kupeleka majumbani mwenu.
v.
Mayahudi wamfahamisha
Mtume maficho ya wenzao:
Katika ngome
hii waislamu walikuta ndani ya nyumba moja iliyokuwa chini ya ardhi zana
kadhaa za kivita. Hizi zilikuwa ni kombeo, vifaru, mavazi ya chuma, majambia
na zana nyingine za kivita ambazo ziliwasaidia sana katika vita hivi. Myahudi
mmoja aliyetekwa na waislamu katika mzingiro wa ngome ya Naaim ndiye aliyewapa
waislamu siri ya ghala hilo la silaha. Huyu alichelea kuuawa na waislamu,
ndipo akaomba kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amani ya maisha yake na ya
familia yake. Mtume akamkubalia, ndipo alipotoboa siri ya mahala
zilipohifadhiwa silaha za Mayahudi katika ngome ya As-swa’ab.
Ngome hii ya As-swa’ab Ibn Muaadh nayo ilipotekwa na waislamu,
Mayahudi wakakimbilia katika ngome ya Az-zubeir. Hii ndio iliyokuwa ngome
madhubuti isiyopenyeka ila kwa taabu na maarifa ya ziada mno, ngome hii
ilikuwa kileleni mwa jabali refu. Waislamu wakaitia mzingironi ngome hii kwa
muda wa siku tatu na Mayahudi wakiendelea kujificha humo bila ya kutoka.
Kukawawia ugumu mno waislamu kuifungua ngome hii mpaka pale Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoambiwa na mmoja wao kuwa kuna kijito cha
maji nyuma ya ngome hiyo. Kijito hiki ndicho kinachoingiza maji ngomeni humo,
Mtume akaamuru kuzibwa kwa kijito kile, ili wakiishiwa na akiba ya maji
walazimike kutoka nje. Na kweli walipoishiwa na akiba ya maji wakawa hawana
njia ila kutoka nje ya ngome, wakapambana kufa kupona mpaka siku hiyo wakauawa
waislamu kadhaa na Mayahudi kumi, huku kukiwa na idadi kubwa ya majeruhi kwa
pande zote mbili. Waislamu wakajibu mashambulizi haya kwa mbinu ya nguvu ya
mtu mmoja mpaka Allah akawapa ushindi wakaiteka na ngome hii. Hii ndio ilikuwa
ngome ya mwisho katika eneo hili la Nitwaah, kutekwa kwa ngome hii
kukamaanisha kuangukia mikononi mwa waislamu eneo lote la Nitwaah. Mayahudi
haoo wakatimkia kwenye eneo la Shiqi, wakaingia katika ngome ya Ubayyi
iliyokuwa juu ya jabali lililoitwa “Shamraan”. Waislamu wakaizingira ngome hii
na kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa Mayahudi. Baada ya mubaraza wa
mashujaa wa pande mbili hizi, waislamu wakaivaa ngome hii wakiongozwa na Abu
Dujaanah Al-Answaariy mpaka wakafanikiwa kupenya ndani. Wapiganaji wa Kiyahudi
waliposhindwa kuhimili nguvu ya waislamu, wakaanza kuparamia kuta kukimbilia
kwenye ngome ya Al-Barii. Humo wakachaga na kutoa upinzani mkali mno. Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaongoza maswahaba wake kuiendea ngome hii.
Watu wa ngome hii walikuwa mahiri mno katika utupaji wa mishale na kuvurumisha
mawe, wakaachia mvua ya mishale na mawe kiasi cha kumpata Mtume wa Allah.
Kutokana na kitisho hiki na mtindo/mbinu hii itumiwayo na Mayahudi, Mtume
akaamuru kulengwa kombeo tayari kuisambaratishia mbali ngome hii. Hili
likawatia khofu kuu Mayahudi wa ngome hii, wakaisalimisha ngome na kutimua
mbio. Kama hivi ndivyo lilivyoangukia mikononi mwa waislamu eneo lote la la
Shiqi kama ilivyokuwa kwa eneo la Nitwaah.
Mayahudi sasa wakaelekea katika eneo lao la mwisho; eneo la
Kutaybah, wakajitia katika ngome ya Qamuuswi ambayo ni ngome ya Banil-Huqayq.
Hii ilikuwa ni miongoni mwa ngome madhubuti mno iliyokuwa chini ya uongozi wa
baadhi ya watukufu wa ukoo huu wa Al-Huqayq. Humo ndimo walimowekwa wanawake
wa ukoo huu, Mtume na maswahaba wake wakaendeleza wimbi la ushindi kwa
kuizingira ngome hii kwa muda wa siku ishirini. Ndipo Allah alipoifungua
kupitia mikono ya Sayyidina Aliy Ibn Abi Twaalib-Allah amuwiye radhi na wote
maswahaba wa Mtume. Lilichukuliwa mateka katika ngome hii, kundi kubwa la
wanawake na watoto, miongoni mwa wanawake hao alikuwemo Bi. Safiyah Bint
Huyay. Huyu aliteuliwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuwa mkewe.
Akamuacha huru na kumuoan, kwa hivyo akawa miongoni mwa mama wa waumini-Allah
awawiye radhi wote.
|